ACHANA na mchecheto wa mashabiki, upepo umebadilika kwa
viongozi, wachezaji mpaka makocha wa Simba na Yanga ambao wakiipigia
hesabu za kiufundi mechi itakayowakutanisha Jumapili, wanasema ni denja
sana.
Simba, ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu
Tanzania Bara inapata kiburi kutokana na ufanisi wa wachezaji wake wa
kigeni pamoja na wazalendo wenye uzoefu.
Wachezaji hao wamekuwa wakichachafya katika kila
mechi ingawa benchi la ufundi limedai inapofika mechi ya watani wa jadi,
mambo huwa ni habari nyingine.
Yanga, ambayo haijafumua kwa kiasi kikubwa kikosi
kilichotwaa ubingwa msimu uliopita, imerudi kwenye fomu na ina ari kubwa
ya kutaka kuishusha Simba kileleni.
Tathimini ya mechi hiyo imekuwa ikizungumziwa zaidi kuanzia kwenye safu ya ulinzi, kiungo na washambuliaji.
Mabeki wa Yanga; Kelvin Yondani ‘Vidic’ na Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ watakuwa na kazi moja tu ya kuzima makali ya Mrundi
Amisi Tambwe mwenye sifa ya kuliona lango kadiri atakavyo.
Tambwe ambaye Simba inamtumia akiwa straika wa
pili baada ya Betram Mwombeki, ana mbinu nyingi za kufunga tena katika
mazingira yoyote, iwe kwa kichwa au mguu.
Madhara yake yanakuwa makubwa zaidi anapocheza na Mwombeki, straika
mrefu mwenye nguvu. Mwombeki anatumiwa na kucheza akiwa straika wa
mwisho ili kuwachosha mabeki na hivyo kumpa urahisi Tambwe kumaliza
kazi.
Mwombeki atakuwa na kazi ya kuhakikisha anacheza
mipira yote ya juu na kumtengenezea Tambwe mipira ya mwisho na inayokufa
ili amalizie jambo ambalo huenda likawatoa jasho Yondani na Cannavaro.
Hata hivyo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Minziro, amewaambia mashabiki wake wasiwe na presha bali waende uwanja kifua mbele.
Wachezaji wengine wa kuogopwa katika kikosi cha
Simba ni mawinga; Haroun Chanongo na Ramadhani Singano ‘Messi’ ambao ni
damu changa.
Kwa upande wa Simba, Mrundi Gilbert Kaze na Joseph Owino raia wa
Uganda wana kazi kwa straika Mrundi Didier Kavumbagu anayesimamishwa
katikati pamoja na Mganda Hamis Kiiza ambaye huwa pembeni kuvizia.
Kavumbagu ambaye ni mrefu na anayemudu pia mipira
ya kichwa, atachezeshwa straika wa mwisho wa kusimama kwa kusudi moja la
kuhakikisha mipira yote mirefu ya kichwa anapiga yeye na si mabeki wa
Simba.
Jukumu lingine la Kavumbagu ni kuwachosha mabeki
kwa sababu ana nguvu. Huwa inapangwa hivyo ili iwe rahisi kwa Kiiza
mwenye umbo la kati aweze kupenya.
Simba itakuwa na tatizo lingine kwa mabeki, Said
Nasor ‘Chollo’ na Haruna Shamte watakaokuwa na kazi ya kuwatuliza,
Mrisho Ngassa na Simon Msuva, ambao ni wajanja na mahiri wa kuhamahama.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’
anasema: “Timu yetu ni bora zaidi ya zote ndiyo maana tunaongoza ligi.
Hao Yanga watake wasitake tutawafunga tu tena kwa mabao mengi, ponea yao
itakuwa ni mabao 3-0.”
Simba imerudi kambini kwenye ufukwe wa Bamba huku Yanga iliyokuwa Kagera ikikamilisha mipango kujichimbia Bagamoyo.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Minziro, anasema:
“Waache Simba watambe, lakini mpira ni dakika 90. Kijumla mechi itakuwa
ngumu kupita maelezo lakini tutashinda.”
Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi, ameshacheza na Simba na Yanga na anasema mchezo huo hautabiriki.
Vikosi
Mwanaspoti imefanya uchunguzi na kugundua kuwa
Simba ya kocha mkuu, Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ anayetumia fomesheni ya
4-4-2 itamwanzisha kipa, Abel Dhaira raia wa Uganda, Cholo atacheza beki
wa kulia, Baba Ubaya atakuwa beki wa kushoto na mabeki wa kati ni Kaze
na Owino.
Jonas Mkude atacheza kiungo mkabaji na Abdulhalim
Humoud ‘Gaucho’ atasimama kiungo mshambuliaji wakati nafasi za winga
zitachezwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ na Chanongo wakati straika ni
Mwombeki na Tambwe.
Mabeki wa kati watakuwa ni Yondani na Cannavaro wakati kiungo mkabaji ni Chuji’ na kiungo mshambuliaji ni Frank Domayo.
Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ atacheza
nafasi ya kiungo wa pembeni kushoto na Ngassa atakuwa kiungo wa kulia.
Mastraika wa katikati ni Kavumbagu na Kiiza.
Mwamuzi wa mchezo
Mwamuzi Israel Nkongo wa Dar es Salaam amepangwa kuchezesha mechi hiyo ya watani wa jadi.
Nkongo, ambaye ni mwamuzi mwenye beji ya Fifa,
alipigwa na wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Stephano Mwasyika na Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, katika mechi ambayo Azam walishinda 3-1 wakati timu
hizo zilipokutana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Machi 10 mwaka
jana.
Nkongo alipata balaa lingine baada ya kuondolewa
dakika za mwisho kuchezesha mechi ya mwisho wa msimu uliopita kati ya
Simba na Yanga, Mei 18 mwaka huu na mechi hiyo ikachezeshwa na Martin
Sanya wa Morogoro.
0 comments: