JE KAULI HII YA WAZIRI WA UJENZI MH.JOHN .P. MAGUFURI ILIKUA SAHIHI AU HEBU SOMA HAPA KWA UNDANI ZAIDI


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amekata mzizi wa fitina, amemfunga kufuli Dk. John Magufuli. Amewaunga mkono wamiliki wa malori ambao wameamua kusitisha mgomo. Lakini watu hawa wana jeuri bwana, eti tena jeuri inayonuka fedha, ziwe zile zilizopatikana kwa njia halali au chafu! Hakuna anayejua, lakini ni fedha zao, hawajavunja benki hawa.

Eti wana jeuri iliyopitiliza, jeuri ya kupimana misuli na waziri wa Serikali, tena hata kwa mambo yaliyo dhahiri kabisa! Eti hawa ni waheshimiwa sana wamiliki wa malori.

Na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kupitia kwa Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli, awali ilikuja juu na kuwawakia wamiliki hawa wa malori kuwa haitabadilisha uamuzi wake wa kufuta msamaha wa tozo kwenye mizani kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya ule uliokubaliwa kisheria.

Eti hii ilikuja baada ya wamiliki wa malori yanayosafirisha mizigo mikoani na nje ya nchi kusitisha kutoa huduma kwa madai kuwa, miongoni mwa mambo mengine, walifikia hatua hiyo “kwa kuchukizwa na kauli ya Dk. Magufuli kuwashutumu kuwa malori yao yanaharibu barabara”. 

Du! Sasa kama malori yakizidisha uzito kwa sababu ya uroho wa kupata faida haraka haraka, kwa kuzidisha uzito, si barabara zitaharibika? Na baada ya kuharibika barabara hizo malori yao hayo yatapita wapi? Na ni nani atagharimia utengenezaji wa barabara hizo? Bila shaka ni kodi za Watanzania, wengi wakiwa walalahoi waliokata tamaa kwa kuzingirwa na umasikini uliokithiri!

Eti sasa wamiliki wa malori haya waachwe wafanye wanavyotaka, waharibu barabara zetu kwa kutaka faida kubwa haraka haraka! Jama jama, marehemu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine, angekuwapo leo wamiliki hawa wa malori wangeikimbia nchi hii!

Huu si ni mzaha, kejeli au matusi kwa Watanzania na Serikali yao? Eti tena ‘vagi’ hii imekuja, kwa mujibu wa Waziri Dk. Magufuli, baada ya uamuzi wa kufuta msamaha wa tozo kutokana na kurekebisha matatizo yaliyokuwapo kwenye mizani nchi nzima, ikiwamo rushwa iliyokuwa imekubuhu. Ya kweli hayo?

Dk. Magufuli hamumunyi maneno. Anasema asilimia 65 ya wafanyakazi kwenye mizani waliokuwa wanashirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu na waadilifu kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, wamefukuzwa kazi na kuajiriwa wengine wapya, ambao nao wanafuatiliwa kwa karibu sana. Kwamba nyuma ya mgomo huu wa wenye malori, eti walikuwa wameshindwa kuwapa rushwa wafanyakazi hawa wapya!

Uamuzi wa kufuta msamaha wa tozo hiyo ulitangazwa na Waziri Dk. Magufuli katika taarifa yake iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa wizara yake, Mussa Iyombe, Oktoba Mosi mwaka huu. Kutokana na kusainiwa kwa taarifa hiyo, magari yote yenye kubeba uzito wa tani 3.5 na kuendelea, yalitakiwa kupimwa bila msamaha wa tozo, na utekelezaji wake ulikuwa uanze rasmi mara baada ya kusainiwa taarifa hiyo.

Kwamba magari yote ambayo yangebainika kuwa yalikuwa yamezidisha uzito, lakini yapo ndani ya asilimia tano ya ule uliokubaliwa kisheria, yalitakiwa ama kupunguza mzigo, kupanga mzigo au kulipia mzigo uliokuwa umezidi mara nne ya tozo ya kawaida kwa mujibu wa sheria na kanuni za barabarani.

Sasa Dk. Magufuli ana ‘bifu’ gani na hawa wenye fedha zao na malori yao kwa kutaka tu barabara za walalahoi zisiharibiwe? Zisiharibiwe ili wakaja kulazimika kuchuna ngozi zao na kutoka jasho ambalo tayari mwilini limekwisha kukakauka kwa madhila mengi wanayokumbana nayo katika kujaribu kuishi ili wagharimie matengenezo ya barabara!

Lakini nchi hii ina vituko! Tofati na majirani zetu, hivi sasa hatuna shirika la ndege la umma! Hatuna reli, tulikwisha kuiua tayari! Sasa tunataka kuua hata barabara zetu! Hivi sisi ni watu wa namna gani? Vizazi vyetu vijavyo vitatupima kwa kutumia vigezo vipi? Hivi tunafurahia kuwa vituko kila kukicha wakati majirani zetu wanatushangaa, kutucheka na kufaidika kupitia ujinga wetu!


Jama jama, nani atatuzindua kutoka kwenye usingizi huu wa pono? Eti duniani kote si mizigo mizito huwa inasafirishwa kwa njia ya reli? Lakini pia na mdomo wa Dk. Magufuli unatakiwa kuwekwa luku. Apime kauli zake kabla ya kuzitoa.
-Mtanzania

0 comments: