UKATILI DAR....!! WAKENYA WAWILI WAMUUA MTANZANIA
Tuesday, 15 October 2013
RAIA wawili wa Kenya, ambao ni ndugu, Mark Ludila (21) na Sila Ludila (16), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kumuua dereva teksi, Ramadhan Hemed (31), mkazi wa Buguruni Malapa, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam. Mauaji hayo yalifanyika hivi karibuni katika eneo la Gymkhana, Wilaya ya Ilala baada ya Wakenya hao kukodi gari ya Hemed aliyekuwa eneo la Feri.
Taarifa zinasema kuwa, watuhumiwa hao baada ya kufika eneo la tukio, walimchoma kisu dereva huyo na kumuua papo hapo.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema watuhumiwa hao walikamatwa na polisi waliokuwa doria.
“Polisi walikuwa doria jirani na eneo la tukio na waliona gari pembeni mwa barabara likiwa limewasha taa zilizowatia wasiwasi.
“Walipolitilia shaka gari hilo, walilifuata na walipofika kwenye gari na kuangalia ndani, waliona kiti cha mbele kikiwa kimetapakaa damu.
“Kwa mbele yao waliwaona watu wawili, walipowahoji walijitambulisha kwa majina lakini pembeni yao kulikuwa na maiti ya dereva waliyokuwa wakitaka kuitupa.
“Walipofanya uchunguzi, walibaini kuwa watu hao ni ndugu na walimkodi dereva huyo hatimaye walipofika katika eneo la tukio walimchoma kisu kwa nia ya kupora gari lake,” alisema Kamanda Kova.
Kwa mujibu wa Kova, watuhumiwa hao watasomewa mashitaka wakati wowote katika Mahakama ya Kisutu.
0 comments: