Si wengi wetu wanaofahamu umuhimu wa kula samaki mara
kwa mara na jinsi kitoweo hiki kilivyo na umuhimu wa kipekee katika afya
ya binadamu
Samaki ni kitoweo ambacho kinatajwa na hata kupendwa na wengi, binadamu au wanyama.
Kitoweo hiki kinaelezwa kuwa na mafuta yenye
kiambata aina ya Omega 3 yanayomfanya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa
kufikiri, kutunza kumbukumbu na kuishi kwa muda mrefu.
Vyakula vyote vinavyozalishwa majini huwa na
kiambata aina ya Omega 3 yenye mafuta yanayotakiwa kwa mwili wa binadamu
yatokanayo na samaki, yana mbegu maalumu zinazomsaidia binadamu katika
ukuaji ambazo pia ni maalumu kwa faida ya mfumo wa ubongo na neva.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wanaoishi
maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na uwezo
mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu
kutokana na kutokuzeeka mapema.
Kwa upande wa Tanzania, watu waliozaliwa na kuishi
maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito ikiwemo kisiwa kama cha
Ukerewe na maeneo mengine karibu na maziwa Victoria, Nyasa, Rukwa hata
visiwani Zanzibar wamebainika kuwa ni watu wenye akili nyingi na
wanaishi kwa muda mrefu ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi
kitakwimu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya Ushauri Nasaha,
Lishe na Afya, Counselnuth, Mary Materu anadhibitisha kuwapo na
virutubisho vingi vinavyopatikana katika kitoweo hiki cha samaki iwapo
wataliwa kwa wakati mwafaka mara tu baada ya kuvuliwa.
“Samaki wana kiambata aina ya Omega 3 ambayo
husaidia katika ukuaji wa binadamu na kujenga ubongo wake vizuri, ndiyo
maana watu wanaoishi katika maeneo yaliyozungukwa na maji mengi
‘bahari, mito au maziwa’ ni watu wenye akili nyingi na watambuzi hata
kama hajaenda shule na akienda shule hufanya vyema sana darasani kama ni
mtoto, angalia watu wanaotoka ukerewe au sehemu nyinginezo,” anasema
Materu.
Materu anafafanua kuwa kinamama wajawazito kwa
upande wao wamekuwa wakipewa ushauri kutumia kitoweo hicho wawapo
wajawazito na kuepuka nyama nyekundu ambayo hata hivyo ni muhimu kwa
mama mjamzito kutumia ili kuongeza damu haraka kwa mjamzito.
“Wajawazito wanapaswa kula samaki kwa wingi ili
kukuza ubongo wa mtoto, pia ni lazima wale nyama nyekundu ili kuongeza
damu kwa uharaka mwilini ila tunawashauri isizidi nusu kilo kwa siku
saba,” anasema Materu na kufafanua umuhimu wa Omega 3 kwa wajawazito.
“Omega 3 humsaidia mtoto kukuza ubongo, kutengeneza retina kwenye mboni ya macho na kutengeneza mfumo wa neva.
Pia, humsaidia mama kuzuia matatizo kama kifafa
cha mimba na sonono baada ya kujifungua. Njia kuu ya mtoto kupata Omega 3
ni kutokana na vyakula anavyokula mama yake.
0 comments: