ZITTO AFICHUA HUJUMA DHIDI YA KATIBA MPYA



NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameibua tuhuma nzito baada ya kudai kuwa kuna njama zinazofanywa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya usiishe.

Alisema lengo la wabunge hao, ni kutaka muda wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 usogezwe mbele hadi 2017, ili waendelee kukaa madarakani.

Kutokana na kuwapo kwa njama hizo, Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema CHADEMA kamwe haikubali uvunjaji wa aina yoyote wa Katiba, huku akimuonya Rais Jakaya Kikwet
e kutothubutu kukubaliana na fitna hizo.


Zitto, alitoa kauli hiyo jana, wakati alipofanya mikutano mbalimbali ya hadhara kwa nyakati tofauti, katika Jimbo la Bukene, mkoani Tabora, kwa ajili ya ujenzi wa chama chake kanda ya magharibi.

Alisema hata vurugu zilizotokea bungeni hivi karibuni na Naibu Spika Job Ndugai, kuruhusu askari kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge kuwakamata na kuwapiga wabunge wa upinzani, ilikuwa sehemu ya mpango huo wa kutaka kusogezwa mbele kwa muda wa wabunge kutoka madarakani.

Alisema hoja inayojengwa na wabunge hao, ambao wameshaanza kuipenyeza kwa ajili ya kumfikia Rais Kikwete, ni kwamba kama Katiba Mpya itapatikana kwa wakati huu, muda wa kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 utakuwa hautoshi.

“Hawa ni wabunge waroho wa madaraka, hawajafanya jambo lolote jema katika majimbo yao, sasa wanajua hawawezi kurudi, ndiyo maana wanataka muda usogezwe ili waendelee kulipwa mshahara na posho …. Sisi CHADEMA, tunasema hilo hapana, hatuwezi kukubali uchaguzi usogezwe kwa miaka miwili na namuonya Rais Kikwete asituhubutu kuingia katika mtego huo unaowahusisha baadhi ya mawaziri,” alisema Zitto.

Alisema wananchi waliwachagua wabunge kwa ajili ya miaka mitano na kwamba kuwapo Katiba Mpya au isiwepo, ni muhimu kwa uchaguzi mkuu ufanyike.

Alisema CHADEMA inatoa kauli hiyo, ili wananchi wajue mkakati huo na washiriki kuupigia kelele, kwa kile alichoeleza kuwa mipango hiyo imeshaanza jijini Dar es Salaam na mjini Dodoma.

Zitto, alisema baadhi ya mawaziri wanataka kutumia nafasi yao ya kuwa karibu na Rais kumshawishi akubali mkakati huo kwa kumueleza kuwa hali hiyo itamjengea heshima na kumbukumbu ya kuiachia nchi Katiba iliyo bora.

Mei 13, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alidai kunasa taarifa za siri za kuwapo kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa madarakani.

Profesa Lipumba, alisema hiyo inatokana na wasiwasi kuwa mchakato wa Katiba Mpya hautaweza kukamilika mwaka 2014, hivyo kutokuwa rahisi kwa uchaguzi kufanyika mwaka 2015.

Profesa Lipumba, alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la CUF.

Hata hivyo, madai hayo ya Profesa Lipumba yalipingwa vikali na Serikali na viongozi wake watatu waandamizi, ambao walijibu walipoulizwa kwa maandishi na mwandishi wetu mjini Dodoma wanakohudhuria kikao cha Bunge.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, alijibu: “Mchakato wa Katiba upo ‘on track’ (unakwenda vizuri) hatuna sababu ya kufanya hivyo.”

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alijibu: “Njooni ofisini kwangu, nitasema ni kitu gani.”


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alijibu kwa utani bila ya kufafanua: “Njooni niwajuze, unajua kamba haitoki Ukambani kama ilivyo kamba.”

0 comments: